Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Test link

SIMULIZI;CHOZI LANGU LITAFUTWA LINI? Sehemu ya 1



MTUNZI:JANE DAVIS
Mahali: Tabora Tanzania.


UTANGULIZI.
Tangu miaka ya zamani mpaka leo hii unyanyasaji wa kijinsia umeshika kasi na kuwa kero kubwa kwa watoto wa kike.Mabinti hawa wamekuwa wakipitia wakati mgumu sana kuanzia majumbani,mitaani na hata mashuleni.
Watoto wa kike wananyanyaswa na kudharauliwa wanageuzwa kuwa chanzo cha mapato kwa kulazimishwa kuolewa ili wazazi wapate mahari.Na wakati mwingine watoto hawa wananyimwa uhuru wa kuongea hisia zao, kujichanganya na marafiki na hata kulazimishwa kushiriki ngono bila ridhaa yao.Mpendwa nisikuchoshe sana ungana nami mtunzi wako Jane Davis usome kisa hiki cha kusikitisha kilichosawili hali halisi inayoendelea katika jamii zetu.
________Songa nayo_____________

"Mamaaa"Aliita mtoto baada ya kuona Mama yake ameshindwa kabisa kutembea na kuamua kukaa chini.
"Uwiii kimbia mwanaaangu, kimbia"Mama alimwambia mwanae huku akitizama mguu wake uliendelea kuvuja damu kutoka kwenye jeraha.
"Jikaze Mama nyanyuka tuondoke"Aliomba mtoto huku akitizama huku na kule kwa hofu.
"Sii siwezi mwanangu, naomba kimbia uondoke niache tu nitakuwa salama"Alijibu huku akijinyonganyonga.
"Hapana Mama watakuua"Alibembeleza mtoto huku akimvuta Mama yake.
"Siwezi mwanangu nahiisi maumivu makali Sana"Alisema huku akimsukuma mwanae aendelee na Safari.
"Siwezi kukuacha Mama heri tufe wote"Alisema mtoto huku akikaa pembeni na Mama yake.
Walikuwa katikati ya pori kubwa lililojaa miti iliyofungamana,vichaka,wadudu na ndege wa kila aina.Ilikuwa ni hatari kuendelea kubaki eneo hilo muda wa usiku kama huo,katika pori hilo kukutana na fisi halikuwa jambo geni,na sio fisi tu bali kulikuwa na mambo ya mauzauza mengi,miezi michache iliyopita kijana mmoja alipotelea porini alipokwenda kukata fito kwa ajili ya ujenzi Lakini hakurejea nyumbani mwezi mzima.Badae alikutwa mtoni Lakini hakuwa na uwezo wa kusikia Wala kuzungumza,mwili wake ulijawa mapele ambapo kila mara alikuwa akijikuna sambamba na kutokwa udenda mdomoni.Mauzauza mengine ikifika usiku ndani ya pori hilo husikika sauti za watu wakicheza ngoma ama harufu ya chakula Lakini hakuna mtu anaeonekana kupika Wala kucheza.
Mama na mwanae walifika pale baada ya kutoroka kijijini kwao, katika kimbiakimbia bahati Mbaya Mama anachomwa na kisiki chenye ncha Kali ambacho kinapenya na kuzama ndani ya unyayo.Anajaribu kukivuta Lakini hafanikiwi kukitoa zaidi ya kuruhusu maumivu na damu nyingi kumtoka.
Kijijini walikotoka walikuwa wakitafutwa kila sehemu.Jopo zima la sungusungu,vijana wa usalama wenye silaha zao za jadi,Kama mkuki,mshale,virungu, mapanga na bakora za mti wa ndati zilizonyooka na kunepanepa hawakusahau tochi kubwa mikononi mwao.Walikuwa wakikimbia mkukumkuku kuelekea ndani ya pori kwa kufuata njia ileile waliyopita mama na mwanae.
"Jamani hivi mna uhakika wanaweza kupita njia hii tusipoteze muda wetu bure."
"Ndio lazima wapite huku wee unadhani watakuwa wapi Sasa."
"Hivi nyie kwa Mawazo yenu mwanamke anaweza kuthubutu kupita porini humu pekeyake?"
"Mwingine hawezi ila kwa huyu Mama anaweza,Kama kaweza kuua mwanae atashindwaje kuwa na ujasiri wa kupita humu?"
"Mmmh maneno yako hayanipi kabisa,mi nafikiri msako ungefanyika nyumba mpaka nyumba Hadi vijiji vya jirani."
"Ni kweli ungeshauri Hilo mapema,kwa Sasa tumeshafika mbali tuendelee tu na Safari".
Sungusungu wale Walikuwa wakibishana baada ya kutembea muda mrefu bila kuona Dalili yoyote ya kuwapata walengwa.Baada ya mabishano ya muda mrefu na hatimae wanakubaliana Ni Bora kuendelea kuwafuata kuliko kurudi nyuma.
***
"Mwanangu jifiche,unaona unaona wanakuja"Mama alimwambia mwanae huku akimuonyesha miali ya mwanga itokanayo na tochi ikija kwa kasi ikimulika kila sehemu.
"Hapana nitakufa na Wewe Mama"Alijibu mtoto bila kuonyesha hofu yoyote.
Mama alimvuta mtoto huku nae akijiburuza kwani hakuweza kutembea kutokana na jeraha la mguuni,wanafanikiwa kuingia kichakani ambapo pembeni yake Kuna mti mkubwa uliostawi vizuri na kujaza majani katika kila tawi lake.
Miale ya tochi ilizidi kusogea na Sasa sungusungu walionekana waziwazi,sauti zao zenye hasira zilisikika vizuri zikitukana na kutoa kejeli kwa Mama huyo.
"Mshenzi huyu tukimpata lazima apate viboko vya kutisha katusumbua Sana"
"Sio viboko ameua na yeye lazima auwawe"
Machozi yanamtoka Baada ya kusikia sentensi hizo,anamkumbatia mwanae kwa nguvu.
"Mama ila Mimi Najua hujaua Ni baba ndio kaua,na wakifika Mimi nitawaambia ukweli."Mtoto anamwambia mama yake ambae Sasa anaacha kumkumbatia.
"Panda juu ya huo mti haraka"Mama anamwambia mwanae anaonyesha kusita,"Panda juu ya mti Kama kweli unapenda niwe hai,Panda nami nitapanda na naomba usitoe sauti yoyote."
Mtoto anapanda juu ya mti,akitegemea na Mama yake atapanda Lakini haikuwa hivyo mama alibaki palepale kwenye kichaka akijikunyata mwili ukimtetemeka.Hazikupita hata dakika 10 tangu mtoto apande juu ya mti sungusungu wakafanikiwa kufika eneo Lile wakifuata Alama ya mburuzo pindi Mama anajiburuza ardhini kuliachia alama na matone ya damu Hilo likawapa mwanga vijana wale waliokuwa Moto Kama wanakwenda kukamata Simba mla watu.
"Maaama"Mtoto anajaribu kuongea Lakini sauti inamezwa na kilio kilichoambatana na kwikwi,anashuhudia Mama yake akipigwa na Kisha bila kupoteza muda wanambeba juu juu kumrudisha kijijini.Hakuna aliyewaza kuhusu mtoto, walijua Ni mama pekee ndiye aliyetoroka.Mtoto anawasindikiza kwa macho mpaka wanatoweka kwenye uoni wake,anajikaza anashuka mtini hofu nyingi inamjaa anawaza arudi nyumbani au asonge mbele.
"Siwezi kurudi nyumbani lazima nisonge mbele heri nife kwa kuliwa na mnyama kuliko kufa kwa mkono wa Baba yangu, mtu mwenye roho Mbaya na tamaa ya mali.Baba asiyependa wanae kupata elimu anachojali yeye Ni kupata Mali,Mali zenyewe anaziteketeza kwenye ulevi wa pombe na kumuacha Mama akiteseka."Aliwaza kichwani mwake huku akinyanyua mguu na kuendelea na Safari.
Mara kwa Mara alijikwaa visiki kutokana na giza,njia nzima alikuwa akimuomba Mungu avuke pori lile salama,hakujua ni wapi anaelekea alichowaza yeye ni popote tu atakapoweza kupata msaada.Alitembea kwa muda kidogo akaanza kuona miti inapungua na Sasa alikutana na mashamba ya watu,alifurahi akijua hivi Karibuni anaweza kuzifikia nyumba za watu aweze kuomba msaada.
"Ipo siku nitarudi kijijini kumkomesha Baba na wote wenye tabia Kama yake"alijisemea pekeake baada ya kukumbuka namna Baba yake alivyokuwa akimshushia kipigo dada yake kwa kosa dogo tu mpaka kumsababishia mauti.Machozi yanamtoka yakipokezana na kamasi nyepesi,anajifuta kwa kutumia gauni lake chakavu na chafu ambalo hakukumbuki hata alilifua lini.
***
Ilikuwa yapata majira ya saa tatu za usiku alionekana binti mdogo akitokea porini na kuishika barabara kubwa ya magari yaendayo mjini Tabora.Umri wake ulikuwa kati ya miaka 12 hadi 13 japokuwa mwili wake ulionekana ni mkubwa.Binti huyo alitembea kwa kuchechemea huku akitizama huku na kule,aliendelea kutembea taratibu huku mara kadhaa akiinama na kushikilia magoti, muda ulivyozidi kwenda ndivyo alivyozidi kuchoka miguu yake ilianza kuuma alitamani kupumzika lakini alihofia usalama wake.Binti akiwa amechoka sana alianza kusikia muungurumo mkubwa ukija nyuma yake aliogopa sana nakutaka kujificha,akageuka aanze kurudi vichakani lakini kabla hajafanya chochote alimulikwa na mwanga mkali usoni.Mwanga huo ukamfanya apoteze uelekeo akipepesuka kidogo Kisha akachuchumaa chini huku akifunika uso wake kwa viganja vya mkono.
ITAENDELEA...

Post a Comment