SEHEMU YA 5
ILIPOISHIA.....
"Heee mbona huli shosti?"Anauliza kwa mshangao lakini rafiki yake hajibu na zaidi amejiinamia kwenye meza.
"Umekuaje Wewe?,au unaumwa Sana?"Anauliza Tena Aisha huku akijaribu kumuinua kichwa,anafanikiwa nakukutana na Hali ambayo hakuidhania meza yote alipolaza kichwa Queen imeenea machozi.Anashtuka zaidi kugundua rafiki yake huyo amepoteza fahamu."Mmmh"Anaguna Aisha,anatoka mbio mpaka ofisini kwa Matroni.
_______SONGA NAYO__________
Aisha alipofika ofisini kwa Matroni,Baada ya salam anaelezea hali ya rafiki yake Queen.Wote pamoja na wanafunzi wengine wawili wanaelekea kwenye kantini ya walimu,wanamkuta Queen akiwa bado hana fahamu.
Matroni anamchunguza kidogo na bila kusema chochote anawapa ishara wambebe,Anatembea kurudi ofisini kwake huku wao wakimfuata kwa nyuma.
Wanaingia nae ofisini kisha kumlaza kitandani,wanamvua viatu na kufungua vishikizo(vifungo) vya shati lake la shule, taratibu Queen anafumbua macho akitizama huku na kule.
"Nendeni nje"Anawaamrisha Nesi na wote wanatoka nje isipokuwa Matroni.
"Unaumwa?"Matroni anamuuliza Queen.
"Hapana,ila kichwa tu kilikuwa kinaniuma hadi nikawa nahisi giza machoni ila sasa hivi nipo sawa."alijibu Queen,na kuonyesha yupo sawa akanyanyuka mwenyewe na kuketi kitandani.
"Jitahidi kunywa maji mengi,hiyo ni dalili ya upungufu wa maji, vilevile Punguza mawazo,weka akili yote kwenye masomo.Si upo kidato cha pili Kuna mtihani wa Taifa miezi michache mbele."Matroni alimpa ushauri.
Queen aliitikia tu ila akili yake haikuwa hapo tena.Alipewa glasi mbili za maji akanywa,akapewa na vidonge vya kutuliza maumivu.Baada ya hapo aliruhusiwa kuondoka kuelekea darasani kuendelea na vipindi Kama kawaida.
"Waooooo,umepona kipenzi changu"Alikuwa Aisha akimpokea Queen,mara tu sura yake ilipotokeza mlangoni mwa darasa,Alikimbia na kumkumbatia kwa nguvu.Darasa zima likaenea sauti za minong'ono.
"Huyo demu mkali balaa, niliumia Sana niliposikia anaumwa,Ujue namzimikia ile kichizi"mwanafunzi mmoja wa kiume alimnong'oneza mwenzake.
"Hahahaha,hivyo vyakula vya walimu Mzee baba usithubutu kugongea namba."Mwanafunzi huyo alimtahadharisha huku akicheka.
"Kwanini,hebu wacha mikwara jomba, lazima nimpige saundi hapa namlia timing tu"Aliongea Kijana huyo aliyedhamiria kumpata mrembo Queen.
"Oyi huwezi kuambulia kitu utakula visiki daily na Mtoto usimpate"Kijana anazidi kumpa tahadhari mwenzake.
Ghafla anaingia mwalimu wa kike akiwa kakunja sura,hata salamu yao haitikii"Wasichana wote mnahitajika hostel haraka"Anamaliza kuongea anageuka na kutoka darasani.
Wasichana wote wanaelekea hostel huku roho zikiwa juu juu, haikuwa kawaida kuitwa hostel muda kama huo,muda wa vipindi ilikuwa lazima Kuna jambo tena jambo kubwa haswa.
"Sijui tunakaguliwa simu!"
"Tunapimwa mimba nini!"
"Hivi leo labda vyoo havijasafishwa"
"Au kuna wageni toka Wizarani?!"
Kila mtu aliwaza kivyake lakini hakuna Aliyekuwa na jibu sahihi.
Walipofika tu hostel walikimbilia mabwenini,wengine walificha simu wengine midoli,huku wengine wakihaha kutandika vizuri vitanda vyao.
"Ngee ngee ngee"Mlio wa kengele uliwakurupusha wanafunzi wote waliokuwa bwenini,walitoka mbio mbio hadi kwenye uwanja mkubwa uliomo ndani ya uwanja ya hostel, uwanja ambao siku zote ulitumika kufanyia sherehe zao ndogo ndogo na mikutano.
Hamadi!, wanafunzi walianza kutetemeka huku wengine wakianza kulia kabisa kwa woga.
Kundi la walimu watano lilijipanga mstari,huku fimbo nyingi zikiwa zimerundikwa chini matitamatita mithili ya mizigo ya kuni.
"Haya mmoja mmoja anapita hapa anapokea zawadi ya chai mbili kisha anaendelea kwa Mwalimu mwingine"Aliongea mwalimu mmoja ambaye alikuwa maarufu kwa namna fimbo zake zilivyokuwa zinauma.Na ukimsumbua anachapa sehemu yoyote.
"Wee nani unalia?!!.Tena naanza na wewe,njoo haraka,hapa shuleni mmekuja kusoma au kufanya Umalaya?!,mnatembea hadi na walimu!"Aliongea kinafiki Mwalimu huyo wa kiume ambaye ndiye kinara wa kulazimisha mapenzi kwa wanafunzi wake.
******
"Lete pochi yangu paaah"Anaongea tena huku akirusha Kofi moja zito shavuni mwa Subi,sekunde tatu kofi la pili linatua kwenye shavu la kulia.Kofi hilo linampeleka Subi chini bila kutarajia.Anaachia ukelele "Mamaaaa"Kisha anatulia kimya.Tayari watu walishajaa kushuhudia tukio hilo,wakisukumana na kukanyagana mithili ya watu wanaogombania chakula.
"Jamani Jamani hebu nipisheni"Anatokea Dada mmoja mtu mzima anajipenyeza kwenye kundi la watu huku akiongea kwa sauti ya juu.
Anawapangua watu hadi anafanikiwa kufika katikati,kitu cha kwanza anamtizama Subi,anamkagua nakugundua amepoteza fahamu haraka anafungua pande moja ya khanga aliyojifunga kiunoni nakuanza kumpepelea.
Wakati huohuo walinzi wanafika,wanawatawanya watu waliokusanyika hapo,wanabaki wachache waliokuwepo awali kabla ya tukio.Anampepelea kidogo Subi anazinduka,anajitahidi kunyanyuka lakini anashindwa anaishia kushika kichwa chake huku akikunja uso.
"Vipi unajisikiaje Mtoto?"Dada anauliza
"Kichwa kinauma Sana"Anajibu Subi.
"Pole sana kitapoa tu"Anaongea Dada kwa sauti ya upole kisha anarudisha macho kwa yule Dada katili aliyempiga Subi.
"Wee binti hivi una akili timamu kweli Wewe,unawezaje kumpiga Mtoto namna hii?"Anaongea huku akimkata jicho kali binti huyo.Ambaye nae hakuwa kimya aliendelea kuporomosha matusi.
"Lazima nimpige na ningemuua leo,kitoto kijizi hiki,akaibie ndugu zake huko sio mimi nitamuua."
"Kwani binti kakuibia nini?"Kijana mmoja anadakia Kisha anaendelea kusema "maana sioni chochote alichonacho Mtoto kuthibitisha kakiiba kwako"
"Kaniibia pochi vilevile kaniibia chipsi na soda wakati nikiwa naongea na simu narudi namkuta anakula chipsi hizo na hicho ndicho kilichonifanya niamini mwizi ni huyu Mtoto,muone sura yake ilivyo Mbaya"Alizidi kuongea huyo binti.
"Huna akili Wewe hapa Stesheni wezi ni wengi, lakini sio huyu Mtoto, huwezi hata kujiuliza hiyo pochi kaificha wapi!"Kijana aliendelea kumpa makavu binti.
"Na Vipi kuhusu chipsi zangu Si amekula."Alikazia binti bila hata chembe ya aibu.
"Binti una roho mbaya wewe kwahiyo upo tayari kuuwa kisa chakula,Tena chipsi tu?,hata kama hali ngumu lakini sio kihivyo."Dada msamaria mwema Aliongea kwa masikitiko.
"Naona una huruma Sana eeh,Sasa mlipie fidia ya alichochukuwa"Binti hakubali kuzipotezea chipsi zake anataka fidia,mmh!.
"Fidia kwa kipi pochi hajachukua,Kama ni chipsi shika hiyo"Aliongea huyo Dada huku akamkabidhi binti noti mpya ya shilingi elfu tano(5000).
Dada alimsaidia Subi kunyanyuka wakaenda kuketi eneo la pembeni kidogo na pale."Nisubiri nikufatie dawa"
Dada anaondoka kuelekea sehemu yenye maduka ya dawa,ananunua dawa,anapitia chakula kwa Mamantilie kisha kurejea alipomuacha Subi.
"Kunywa hizi dawa kichwa kitapoa Mara moja"Anamkabidhi Subi dawa na chupa ya maji,anatafuna na kunywa maji bila uoga.Baada ya hapo akapewa chakula ilikuwa ni wali maharage na mchicha.Subi akaanza kula chakula kile kwa pupa kwani njaa ilikuwa imemshika haswa.Alikula chakula chote bila kuachia hata punje,akanywa na maji ya kutosha,Sasa alijihisi mwenye nguvu.
"Asante kwa chakula"Alishukuru Subi.
"Usijali,Mimi naitwa Upendo,Wewe Je?"Aliongea Dada Upendo, mwanamke mwenye roho nzuri iliyojaa Upendo kama jina lake lilivyo.
"Naitwa Subi au Subira," Alijibu Subi hakuacha kitu alieleza yote yaliyomsibu,Alijieleza wazi yupo peke yake na yupo pale kutafuta msaada au hata kazi yoyote kutokana na matatizo aliyokimbia kijijini kwao.Alieleza yote kisha akaanza kulia kwa uchungu akimsihi Dada Upendo amsaidie kwa namna yoyote ile.
"Nyamaza usilie kabisa kila kitu kitakuwa sawa"Upendo Aliongea huku akimfuta machozi,kiukweli toka moyoni mwake alimuonea huruma sana.
"Sijui nimuache nyumbani,ila watamsumbua Sana"alikuwa akiwaza amuache nyumbani kwao, lakini nyumbani hapo walibaki vijana wa kiume pekee.Hali hiyo ikamfanya asite uamuzi huo kuhofia usumbufu wowote kwa binti huyo.
Akiwa anawaza mara wazo likamjia,akafungua pochi akatoa simu,akatoa lock,akabonyeza menu akaelekea kwenye majina akatafuta moja kwa moja akagusa jina"Dada Neema" akabofya kuipiga kisha akaiweka simu sikioni.
Je Subi atapata msaada? Usikose sehemu ijayo.Itaendelea.