Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipiscing elit. Test link

SIMULIZI: CHOZI LANGU LITAFUTWA LINI? sehemu ya 6

SEHEMU YA 6



ILIPOISHIA.....

"Sijui nimuache nyumbani,ila watamsumbua Sana"alikuwa akiwaza amuache nyumbani kwao, lakini nyumbani hapo walibaki vijana wa kiume pekee.Hali hiyo ikamfanya asite uamuzi huo kuhofia usumbufu wowote kwa binti huyo.

Akiwa anawaza mara wazo likamjia,akafungua pochi akatoa simu,akatoa lock,akabonyeza menu akaelekea kwenye majina akatafuta moja kwa moja akagusa jina"Dada Neema" akabofya kuipiga kisha akaiweka simu sikioni.

________SONGA NAYO_____________

"Hello, salama Dada za huko?"

"Huku kwema pia,Vipi ushaanza kwenda kazini?"

"Hee bado hujapata tu,basi naomba nikuletee huyu mwanangu"

"Ndio,Leo usiku ila mie nitaishia chuoni."

"Usijali,atafika tu kikubwa msubirie stendi na simu yako iwe hewani."

"Haya Asante sana, likizo nitamfuata"

Dada Upendo alikuwa anaongea na simu na baada ya kumaliza akaanza kumwambia Subi.
"Mimi siwezi kukupa kazi mdogo wangu kwani bado nipo masomoni,ninasoma na hivi naelekea chuoni Dodoma.Lakini nina dada yangu yuko Daresalam anatafuta msaidizi wa kulea mtoto je utaweza?"

"Ndio dada ninaweza"alijibu kwa haraka Subi.

"Sawa tunasafiri pamoja lakini mimi nitaishia Dodoma.Najua hujawahi kufika Dar hivyo kwa treni utahangaika tukishuka Dodoma nitakupakia kwenye Basi nitakupa na hii simu ndogo ukifika tu stendi unampigia simu dada atakuwepo hapo kukupokea.si unajua kusoma?

"Ndio"Subi aliitikia.

*****
"Jamani Nyoka, nyoka huyo"

"Mamaa nyoka,msaada Jamani"

Zilikuwa ni kelele za watu baada ya kumuona nyoka mkubwa mweusi mwenye mabaka meupe huku akiwa amevishwa shanga nyekundu.Ilikuwa ni ajabu sana,tena ajabu ya mwaka kwa kiumbe huyo kuonekana Stesheni hapo.

Wasafiri walichanganyikiwa kila mtu Alikimbia kivyake kuokoa uhai wake,watu walikanyagana,wenye presha wakianguka na kuzimia,wenye watoto kila mtu alibagaa mwanae huku wengine wakikimbia mizigo yao.

Lakini Nyoka huyo alitoweka kimaajabu,hata walinzi na wanausalama wa hapo Stesheni wasijue amekimbilia wapi.
Huku wakihisi huenda wamejichanganya tu hakukuwa na Nyoka yoyote.Basi waliwatuliza wasafiri hao na hali ya Amani ikarejea.

Hali ilikuwa mbaya upande wa Subi, wakati kelele za watu wakisema nyoka,alipozisikia tu kumbukumbu zinamkumbusha porini aliponusurika kubakwa na Mzee,picha ya Lile joka inamjia anajikuta anakimbia hovyohovyo Kama mtu aliyechanganyikiwa huku akimuita Mama yake.
Sasa Hali ilikuwa shwari watu walitulia,nae akapumua kidogo lakini alishangaa kujikuta yupo sehemu nyingine tofauti kabisa na pale alipokuwa ameketi mwanzo.

Anashtuka Sana,anageuka kutazama huku na kule Kama atamuona Dada Upendo, lakini hakumuona.Alianza kuzunguka humo Stesheni lakini hakumtia machoni.Na kwa vile ilikuwa ni usiku ugumu ukaongezeka kwake.Alikodoa na kukodoa macho amuone wapi!! 
Hadi muda wa Treni kuondoka ukawadia,na kwa macho yake alishuhudia ikipiga honi ya kwaheri kisha kuondoka kwa mwendo wa madaha mfano wa jongoo.

Michirizi miyembamba ya machozi ikajichora kuanzia machoni ikitiririka hadi mashavuni, alikuwa akilia,alilia sana nani amjali?.Kila.mtu alimpita tu akidhani huenda ni chizi.Tumaini lilimkimbia sauti ikamkauka akabaki akilia kwa kwikwi akiwa amejikunyata mithili ya kifaranga cha kuku kilichotelekezwa na mamaye.

Alikaa hapo stesheni mpaka asubuhi ndipo alipoamua kuondoka.hakuwa na sehemu ya kwenda hivyo alibaki akizulula tu huku na huko alikata vichochoro hatimaye akatokeza kwenye barabara ya lami upande wa mkono wake wa kushoto kulikuwa na uwanja mkubwa wa mpira sambamba na majengo mengi mengi yenye rangi ya damu ya Mzee na nyeupe.Upande wa mkono wake wa kulia nako kulikuwa na majengo ambayo hayakuwa mazuri Kama ya upande wa kushoto.

Mbele kulikuwa na barabara ya vumbi kwa kuwa aliogopa pikipiki na magari mengi yaliyokuwa yakipita kwenye barabara ya lami,akaamua kuachana nayo na kufuata barabara yenye vumbi.
Alitembea akipita nyuma ya jengo kubwa ambapo aliona wanafunzi wengi wa kike wakifua unifomu zao za shule, ilikuwa ni Hostel ya shule ya sekondari Kazima.

Akaenda mbele kidogo akakutana na kibao kilichosomeka sawia"Shule ya Msingi Uhuru", pamoja na kusitisha masomo akiwa darasa la tatu tu, lakini mtoto huyo alifahamu kuandika, kusoma na kuhesabu.Na hicho ndicho akichofaidika shuleni.

Baada ya kusoma maandishi hayo alikumbuka Maisha ya shule alitamani Sana kurudi shule,moyo wake ulizidi kumuuma pale alipowaona wanafunzi wa rika lake waliovalia sketi za rangi ya kijani zenye marinda makubwa yaliyolalia upande mmoja,shati nyeupe kwa juu, mgongoni walibeba begi nzuri zenye michoro michoro na chini walistiri miguu yao kwa raba na soksi ndefu nyeupe,hakika walipendeza unifomu hizo nadhifu.


Taratibu Subi akaanza kuwafuata watoto hao waliokuwa wakinunua visheti kwa Mama mmoja muda huo wa pumziko.Alijaribu kuwaomba Lakini walimkimbia wakidhani ni chizi kulingana na mavazi yake machafu.
Pembeni kulikuwa na mabinti wakicheza mdako aliwafuata nakuomba kucheza nao pia walimzuia isipokuwa mmoja yeye alimuomba wacheze nae walicheza huku wakiongea.

"Unaitwa nani?,Mimi naitwa Tina"

"Naitwa Subi au Subira"

"Subira yavuta heri, kumbe ndiye wewe, mwalimu alitufundisha,wewe mbona hausomi au hupendi shule?"

"Napenda Sana ila Sina wa kuninunulia nguo za shule"

"Baba yako je, kwani kwenu wapi?"

"Baba hataki nisome,anatupiga anataka tuolewe,kwetu kijijini nimekimbia"

"Mmmh!, Usirudi na usikubali kabisa.Mwalimu Alisema marufuku watoto kuolewa,hata Raisi,unamjua Raisi wa Tanzania?"

"Hapana"

"Kasema marufuku watoto kuolewa,ngoja nikuonyeshe picha yake huyu hapa,ona ona na jina lake Hilo soma hapo chini"
"Mheshimiwa Jo..hn Po..mbe..Ma.gu...Alisoma Subi kwa kusuasua.

DOWNLOAD HERE

Hayo yalikuwa maongezi ya Subi na rafiki yake mpya Tina,waliongea mengi Subi alieleza bayana kuwa anapenda kusoma lakini hana mtu wakumnunulia nguo za shule,na zaidi Baba yake anataka aolewe.Tina anamshauri asikubali huku akimwambia yeye ana shangazi yake atampeleka amnunulie nguo za shule na atasoma bila shida.

Kengele iligongwa wanafunzi wakaingia madarasani,Subi alibaki ameketi chini ya mti akimsubiri Tina.Hatimaye mida ya kutoka shule ikafika,baada ya kuagwa wakaongozana kuelekea nyumbani kwao Tina.

Hakukuwa na umbali mrefu toka shuleni mpaka nyumbani kwao Tina..Wanafika kwenye nyumba hiyo,Tina anagonga mlinzi anamfungulia,anashangaa kumuona binti mwingine nyuma lakini anashindwa kuuliza chochote kwa kuwa si kazi yake.

Subi anaanza kuishangaa nyumba hiyo,Ni nyumba yenye mandhari nzuri, uwanja mpana,bustsni ya Maua,bwawa la kuogelea,ni vitu vipya ambavyo hakuwahi kuviona popote.Tina anamuongoza Subi mpaka ndani sebuleni.

"Kaa hapo usiogope Aunt yangu hata sio mkali,"Tina anamwambia Subi ambaye alionyesha wazi kuogopa kukaa mule ndani kulimokuwa na samani za bei ghali ambazo hakuwahi kuziona katika maisha yake tangu azaliwe.

"Aunt nimekuja na mgeni"Tina anapaza sauti kumuita shangazi yake ambaye anamsikia vyema akiwa jikoni anatoka mpaka sebuleni macho yake yanatua moja kwa moja kwa Subi aliyekaa juu ya sofa.

Je unadhani Subi atapokelewa?,Vipi kumrudisha shuleni?
Usikose sehemu ijayo..ITAENDELEA.....

Post a Comment